Watu 200 wafariki kwenye maporomoko ya mgodi DRC

Tom Mathinji
2 Min Read
Watu 200 wafariki kwenye maporomoko ya mgodi nchini DRC.

Taarifa na BBC

Serikali ya Jamhuri ya demokrasia ya Congo imesema zaidi ya watu 200 wamefariki, wakiwemo watoto 70, baada ya maporomoko ya ardhi mashariki mwa nchi hiyo.

Maporomoko hayo yalitokea katika eneo la Rubaya, ambalo ndilo chanzo kikubwa cha madini ya coltan nchini humo.

Tukio hilo lilitokea Jumanne baada ya mvua kubwa kunyesha katika eneo hilo ambalo linadhibitiwa na waasi.

Katika taarifa ya wizara ya madini ililaumu kundi la waasi la M23, ikisema wanaruhusu uchimbaji wa madini kinyume cha sheria bila kufuata viwango vya usalama.

Kundi la M23 bado halijatoa kauli yoyote kuhusu tukio hilo. Hata hivyo, chanzo kimoja kutoka Rubaya kilisema kuwa kuporomoka huko kwa mgodi kulisababishwa na mashambulizi kutoka kwa majeshi ya serikali, na kwamba watu sita tu ndio waliokufa. Hata hivyo serikali bado haijajibu madai hayo.

Migodi ya Rubaya inaaminika kuwa na takribani asilimia 15 ya akiba ya coltan duniani, na karibu nusu ya akiba yote ya madini hayo nchini DR Congo.

Tangu mwaka 2024, waasi wa M23 wamekuwa wakidhibiti eneo la Rubaya, lililoko takribani kilomita 70 magharibi mwa mji wa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu kaskazini.

Mamlaka zilisema juhudi za uokoaji baada ya maporomoko ya Jumanne zilikwama kutokana na hali hatari katika eneo hilo. Serikali pia iliilaumu kundi la waasi kwa kuweka vikwazo kwa raia, jambo lililofanya shughuli za uokoaji kuwa ngumu.

Wizara ya madini iliongeza kuwa kukosekana kwa usimamizi rasmi katika mgodi huo kumewaacha wachimbaji bila ulinzi wa msingi wa usalama kazini.

TAGGED:
Share This Article