Watu wawili wamethibitishwa kufariki kutokana na shambulizi lililotekelezwa na wanaoshukiwa kuwa magaidi waliowashambulia wasafiri kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garisen katika eneo la Lango la Simba karibu na mpaka wa kaunti za Lamu na Tana River.
Mtu mmoja aliyekuwa na majeraha yaliyotishia maisha alifariki wakati akikimbizwa hospitalini ili kupewa matibabu ya dharura.
Watu wengine wapatao 10 walijeruhiwa wakati wa shambulizi hilo huku wengine ambao idadi yao bado haijabainika wakiwa hawajulikani walipo.
Katika taarifa aliyoitoa leo Jumanne, Waziri wa Usalama wa Taifa Kithure Kindiki anasema maafisa wa usalama waliitikia haraka shambulizi hilo.
“Maafisa wa usalama kutoka kambi ya Nyangoro waliokuwa wakishika doria kwenye barabara hiyo waliitikia haraka na makabiliano na magaidi hao wanaokadiriwa kuwa 60 kuzuka na kuwalazimu kukimbilia msitu wa Boni,” amesema Waziri Kindiki.
“Huku operesheni ya usalama inayowahusisha maafisa kutoka Huduma ya Taifa ya Polisi na wanajeshi wa KDF ikiendelea kwa sasa, majeruhi wanaendelea kutibiwa na msako wa kuwatafuta na kuwaokoa wasiojulikana walipo pia unaendelea.”
Kaunti ya Lamu imeshuhudia visa vya ukosefu wa usalama siku zilizopita na ambavyo nyakati nyingine vimesababisha vifo na uharibifu wa mali.
Visa hivyo vinashukiwa kutekelezwa na kundi la wanamgambo la Al-shabaab.