Idadi ya waliofariki nchini kutokana na mvua ya masika inayoendelea kushuhudiwa katika pembe mbalimbali imefikia 179.
Msemaji wa serikali Isaac Mwaura alisema kuwa miili kumi ilipatikana siku ya Jumatano katika visa tofauti vya watu kusombwa na mafuriko au kuzama kwenye maji na kujumlisha 179.
Kaunti ya Machakos pekee iliripoti vifo vinne kutokana na mafuriko siku ya Jumatano.
Watu wanne waliripotowa kuaga dunia katika kaunti ndogo ya Matungulu kaunti ya Machakos, ikiwemo mama na mjukuu wake wa kiume waliotumbukia kwenye choo kilichokuwa kikikarabatiwa walipokuwa wakikagua .
Pia mtu mmoja alifariki katika kijiji cha Kyandili eneo la Kangundo, wakati nyumba alimokuwa amelala iliposombwa na maji, huku mvulana mmoja wa umri wa miaka mitano katika eneo la Katani akizama maji alipokuwa akicheza na wenzake.