Watu wapatao 15 waliuawa na wengine wengi kuachwa na majeraha huko New Orleans, nchini Marekani baada ya mwanaume mmoja kuwagonga kwa gari lake walipokuwa wakisherehekea mwaka mpya.
Maafisa wa usalama nchini humo wametaja kisa hicho kuwa shambulizi la kigaidi na kulihusisha na kundi la ISIL (ISIS).
Rais wa Marekani Joe Biden alisema kwamba shirika la uchunguzi la Marekani FBI lilimfahamisha kwamba mshukiwa wa shambulizi hilo alikuwa amechapisha video fulani katika mitandao ya kijamii zilizoashiria kwamba alikuwa anamotishwa na kundi hilo lililojihami la mashariki ya kati.
Kiongozi huyo alihakikishia wakazi wa New Orleans kwamba anasimama nao wanapoomboleza, taarifa aliyotoa kutoka kwa makazi ya rais ya likizo ya Camp David.
Biden alisema pia kwamba maafisa wanachunguza pia mlipuko wa gari aina ya Tesla Cybertruck nje ya hoteli inayomilikiwa na Rais mteule Donald Trump huko Las Vegas.
Shirika la FBI liliripoti kwamba haliamini mshukiwa mkuu wa shambulizi hilo Shamsud-Din Jabbar, wa miaka 42 alikuwa anafanya kazi peke yake na kwamba walipata bendera ya ISILkwenye gari lake.
Alethea Duncan, anayesimamia tawi la New Orleans la FBI amesema wanafanya kila wawezalo kuchunguza uhusiano wa mshukiwa na makundi ya kigaidi.
Duncan alisema pia kwamba vilipuzi vya kutengenezwa nyumbani vilipatikana katika eneo fulani la jiji hilo lakini viliharibiwa.
Shambulizi hilo lilitekelezwa Jumatano saa tisa na dakika 15 alfajiri saa za Marekani karibu na makutano ya barabara za Canal na Bourbon zinazotumiwa sana na wanaotembea kwa miguu.