Watu wapatao 124 wamefariki baada ya ndege ya abiria kushika moto ilipoteleza na kuondoka kwenye njia yake wakati wa kutua katika uwanja wa ndege mjini Muan nchini Korea Kusini.
Ajali hiyo ilitokea saa tatu na dakika tatu za asubuhi kulingana na saa za nchi hiyo leo Jumapili.
Ndege hiyo ya Jeju ilikuwa imebeba abiria 175 na wahudumu sita kutoka jiji kuu la Thailand Bangkok, na ilitua katika uwanja wa kimataifa wa Muan umbali wa kilomita 289 kusini magharibi mwa jiji kuu la Seoul.
Shirika la kitaifa la zima moto nchini humo lilithibitisha kwamba watu 124, wanawake 57, wanaume 54 na 13 ambao jinsia haikubainika mara moja waliangamia kwenye ajali hiyo.
Watu wawili ambao wote ni wahudumu wa ndege hiyo waliokolewa na moto huo umezimwa.
Wahudumu wa zima moto, waliozungumza na shirika la habari la Yonhap wanasema kwamba matumaini ya kupata manusura zaidi ni finyu.
Mwanahabari wa Al Jazeera Rob McBride anasema huenda kulikuwa na hitilafu kwenye gia ya kutua na picha zilizosambazwa mitandaoni zinaonyesha ndege hiyo ikitua kwa tumbo lake na kuteleza kwenye njia yake kabla ya kulipuka.
Ndege hiyo inaaminika kuwa na abiria wawili raia wa Thailand huku wengine wote wakiaminika kuwa raia wa Korea Kusini.