Watu 12 wafariki kwenye ajali ya barabarani Chuka

Marion Bosire
1 Min Read

Watu 12 walifariki kwenye ajali ya barabarani liyohusisha magari mawili kwenye barabara kutoka Chuka kuelekea Meru katika daraja ya mto Nithi, kaunti ya Tharaka Nithi.

Kulingana na taarifa ya polisi wa kituo kidogo cha Trafiki cha Chogoria, ajali hiyo ilitokea jana jioni saa moja na dakika ishirini .

Gari aina ya Toyota Hiace iliyokuwa ikielekea Chuka General nambari ya usajili KDN 532V iliyokuwa ikiendeshwa na dereva ambaye hajatambuliwa iligongana ana kwa ana na gari nyingine aina ya Pick Up nambari ya usajili KDC 636G iliyokuwa ikielekea Meru.

Dereva wa gari la Hiace anasemekana kuondoka kwenye upande wake wa barabara ndiposa ikagongana na hiyo nyingine.

Wote waliokuwa kwenye gari hilo ambao ni wanawake wanane, wanaume wawili na watoto wawili hawajatambuliwa.

Dereva wa Pick Up aitwaye Martin Kirimi Mugambi alijeruhiwa mguu wa kulia huku Wanjiku Kimau akiumia kichwa.

Wawili hao walipelekwa kwenye hospitali ya rufaa ya Chuka kwa matibabu na miili ya waathiriwa imepelekwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali hiyo.

Miili hiyo inasubiri uchunguzi na utambuzi.

Magari hayo mawili ambayo yaliharibia sana yamebururwa hadi kituo cha polisi cha Chogoria.

Share This Article