Takriban watu 100 wamefariki na wengine 150 kujeruhiwa, baada ya moto kuzuka kwenye harusi kaskazini mwa Iraq, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti.
Akizungumza na wanahabari hapo awali, naibu mkurugenzi mkuu wa afya Ahmed Dubardani, aliongeza kuwa takriban watu hamsini wako katika hali mbaya.
“Wengi wa waliojeruhiwa waliungua kabisa. Na wengine asilimia 50 hadi 60 ya miili yao iliungua. Hali hiyo si nzuri hata kidogo,” alisema.
Aidha aliongeza kuwa wengi wa waliojeruhiwa walikuwa vijana wa kiume na wa kike na hadi kufikia wakati alikuwa akitoa taarifa hiyo, hakuna aliyekuwa ameruhusiwa kuondoka hospitali.
Maafisa nchini Iraq wamesema uchunguzi wa awali unaashiria kuwa moto huo ulitokana na fataki zilizowashwa ndani ya ukumbi katika wilaya ya Qaraqosh.