Watu wasiopungua 10 waliuawa juzi Jumatano katika shambulizi la
ufyatuaji risasi lililofanyika nchini Montenegro.
Ripoti zinaashiria kuwa mwanamume mmoja alifaytua risasi
Jumatano alasiri kwenye mgahawa mmoja uliopo katika mji mdogo
magharibi mwa nchi hiyo.
Kisha mwanamume huyo alielekea maeneo mengine matatu na kuendelea
na mashambulizi yake ya ufyatuaji risasi.
Miongoni mwa waliofariki ni mmiliki wa baa na wanawe wawili. Watu wengine wanne walijeruhiwa vibaya.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 45, alijaribu kujiua karibu na nyumbani kwake baada ya kubanwa na
polisi lakini baadaye alithibitishwa kufariki.
Kusudi la mauaji hayo na taarifa zingine za kina haziajawekwa bayana.
Hata hivyo, polisi wanasema mshukiwa alidhaniwa kulewa chakari na
kulikuwa na mivutano kabla ya kufyatuliwa kwa risasi.
Rais wa Montenegro Jakov Milatovic amesema “alishtushwa na kupigwa na bumbuazi” na kwamba “amehuzunika kufuatia vifo
vya watu wasiokuwa na hatia.”
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Milojko Spajic amesema mamlaka
zitatilia maanani kuimarisha vigezo vya kumiliki na kubeba silaha nchini humo.