Watu kumi wamekamatwa katika msako dhidi ya pombe haramu katika kaunti ya Homa Bay.
Kamati ya usalama na ujasusi katika kaunti hiyo ikiongozwa na kamishna wa kaunti Moses Lilan, ilitekeleza msako huo leo Jumanne katika kijiji cha Nyambare na kukamata watu hao.
Hii ni baada ya kufahamishwa na wananchi kuhusu utayarishaji na uuzaji wa pombe haramu ambao umekuwa ukiendelea katika fuo za mto Rangwe kijijini humo.
Wakati wa msako huo, lita 11,500 za pombe aina ya kangara, lita 1,000 za chang’aa na vifaa vya kutayarisha pombe vilitwaliwa na maafisa hao wa usalama.
Washukiwa waliokamatwa walipelekwa katika kituo cha polisi cha Homa Bay na baadaye wakapelekwa mahakamani kujibu mashtaka dhidi yao.