Botswana, Msumbiji, na Tanzania zilikuwa timu tatu za mwisho kujikatia tiketi kwa kindumbwendumbwe cha kuwania kombe la mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka ujao nchini Morocco baada ya kukamilika kwa mechi za makundi za kufuzu Jumanne usiku.
The Zebras ya Botswana ilifuzu baada ya kumaliza ya pili kundini C kufuatia sare ya bao moja dhidi ya wenyeji Misri katika mechi ya mwisho.
Botswana watakuwa wakicheza AFCON kwa mara ya pili baada ya kushiriki kwa mara ya mwisho mwaka 2022.
Mambas ya Msumbiji iliwashinda Guinea Bissau mabao 2-1 katika kundi I na kufuzu kwa jumla ya pointi 11.
Msumbiji watakuwa wakishiriki AFCON ya sita kwa jumla na ya pili kwa mpigo.
Taifa Stars ya Tanzania ilifuzu baada ya kuwashinda Guinea bao moja kwa bila ugani Benjamin Mkapa na kumaliza ya pili nyuma ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Taifa Stars watakuwa wakishiriki AFCON kwa mara ya pili mtawalia baada ya kumaliza nafasi ya tatu katika hatua ya makundi kwenye makala ya mapema mwaka huu nchini Ivory Coast.
Orodha kamili ya mataifa 24 yaliyofuzu kwa kipute cha AFCON mwaka ujao ni pamoja na wenyeji Morocco, Burkina Faso, Cameroon, Algeria, DR Congo, Senegal, Egypt, Angola, na Equatorial Guinea.
Timu nyingine ni Côte d’Ivoire, Uganda, South Africa, Gabon, Tunisia, Nigeria, Zambia, Mali.
Zimbabwe, Comoros, Sudan, Benin, Tanzania, Mozambique na Botswana pia zimefuzu.
Morocco watakuwa wenyeji wa makala ya 35 ya AFCON kati ya Disemba 21 mwaka 2025 na Januari 18 mwaka 2026.