Watoto wanne wameuawa kwa kudungwa kisu katika shule moja ya chekechea Jijini Kampala nchini Uganda.
Kulingana na idara ya Polisi nchini humo, watoto hao ambao ni wavulana watatu na msichana mmoja, wana kati ya umri wa miaka miwili na maka minne.
Watoto hao walitambuliwa kuwa Eteku Gideon, Kaise Alungat, Ignatius Sserwange na Ryan Odeke,
Kupitia kwa ukurasa wa X, polisi walithibitisha kumkamata mshukiwa wa mauaji hayo kwenye eneo la tukio, wakidokeza kuwa huenda alitumia zaidi ya kisu kimoja kuwashambulia watoto hao.
“Maafisa wa polisi walifanikiwa kumkamata mshukiwa ambaye alitambuliwa kuwa Okello Christopher Onyu mwenye umri wa miaka 39,” ilisema Idara hiyo ya polisi.
Polisi walisema mshukiwa huyo anahojiwa huku uchunguzi wa kisa hicho ukiendelea kubaini chanzo chake.