Watoto 15 waokolewa kutoka maeneo yaliyofurika Tana River

Marion Bosire
1 Min Read

Shirika la msalaba mwekundu Jumanne liliokoa watoto 15 kutoka kwenye mashamba wakati ambapo mafuriko yanaendelea kusababisha uharibifu katika kaunti ya Tana River.

Watoto hao wa chini ya umri wa miaka 10 walikuwa na wazazi wao kwenye mashamba hayo ya ndizi, mahindi na maembe wakati mashamba hayo yalizingirwa na maji ya mafuriko na ikawa vigumu kwao kufikia maeneo salama.

Inaaminika kwamba walisusia miito ya kuhamia maeneo salama kwa sababu ya mazao yao mashambani na hata hivyo waliweza kuokoa tu kiwango kidogo.

Wakazi wa eneo la Feji huko Garsen waliomba usaidizi kutoka kwa shirika la msalaba mwekundu na wafanyakazi wa shirika hilo wakatafuta mashua na kuanza shughuli ya uokoaji.

Wanawake watatu na mwanaume mmoja waliokolewa pia kwenye oparesheni hiyo kulingana na meneja wa shirika la Red Cross eneo la Pwani Hassan Musa.

Kila mara mto Tana unapovunja kingo zake kutokana na mvua kubwa huko Tana Kaskazini Madogo maji yote huteremka chini na kusababisha madhara katika eneo la Tana Delta.

Wafanyakazi hao wa Red Cross walichukua dakika 45 kufikia waliokuwa wameomba msaada kwa kutumia mashua na wakielekewa huko walikutana na mashua nyingine zikiwa zimebeba watu.

Maji hayo yalionekana kuongezeka kila mara huku wakazi wa maeneo hayo wakishauriwa kuhamia maeneo salama.

Share This Article