Baraza la Sanaa la Taifa nchini Tanzania ambalo liko chini ya wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo limetangaza shindano la kuunda mdundo wa taifa.
Katika taarifa rasmi, katibu mtendaji wa BASATA Kedmon Mapana alielezea kwamba tayari wamepata vionjo zaidi ya 400, vya watayarishaji muziki mbali mbali nchini Tanzania.
Alisema chini ya mpango wa mdundo wa taifa, baraza limeandaa shindano la watayarishaji muziki yaani “music Producers” lenye lengo la kuwahamasisha kuzalisha ngoma mbalimbali zinazotumia vionjo vya asili ya Tanzania.
Mapana alielezea kwamba wanataka ngoma itakayotengenezwa iwe inachezeka na kutoa hamasa.
“Kila mtayarishaji muziki awasilishe ngoma moja kupitia mfumo wa wadau wa sanaa (AMIS) unaopatikana katika kiungo https:lsanaa.go.tz kuanzia tarehe 20 Disemba hadi 30 Disemba, 2024.” alisema Mapana kwenye taarifa hiyo.
Watayarishaji muziki ambao wanakubaliwa kuingia kwenye shindano hilo ni wale ambao usajili wao kwenye BASATA uko sawa au waliosajiliwa kwenye baraza la Sanaa na Sensa ya Filamu, Zanzibar (BASSF).
Mshindi wa kwanza wa shindano hilo atatuzwa shilingi milioni saba pesa za Tanzania, wa pili atuzwe shilingi milioni tatu huku wa tatu akinyakua shilingi milioni mbili.