Mahakama ya Malindi imewahukumu wanaume watatu miaka 15 gerezani kila mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya kumjeruhi mwanahabari Alex Kalama Gona eneo hilo la Malindi.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mkuu Mwandamizi James Ongondo alisema kuwa Kennedy Makau Kazungu, Anderson Kazungu Makau na Justine Kazungu Makau walimvamia Kalama kwa vifaa butu nyumbani kwake.
Kalama alieleza mahakama kuwa “nilikuwa nimeinama kufungua mfereji uliofungika waliponivamia. Kennedy alinipiga kichwani kwa nyundo nao Anderson na Justine wakanipiga mbavu na sehemu nyingine za mwili. Jackson Kumbeja akiwa hotelini alisikia uyowe wangu na akaja kuniokoa.’’
Kwa upande wake, Kumbeja alieleza mahakama kuwa,”Nilipofika sehemu ya tukio, Gona alikuwa amevamiwa na watatu hao. Nilimuona Kennedy akimpiga kwa nyundo kichwani na kuampa kummaliza nao wengine wakimpiga kwa magogo wakati akijaribu kutoroka.”
Kumbeja alizidi kueleza kuwa alimsaidia Kalama hadi kwa karakana iliyokuwa karibu ambapo walipata pikipiki iliyowapeleka hospitalini na baadaye kwenye kituo cha polisi ambapo walipiga ripoti.
Ripoti ya matibabu iliyowasilishwa mahakamani na Dkt. Rimba, ilieleza kuwa mhasiriwa alikatwa vibaya kichwani na pia alipata majeraha kwenye fuvu la kichwa hali iliyosababisha kulazwa kuanzia Octoba 31,2022 hadi Novemba 4,2022.
Hata hivyo, wakili wa watatu hao Allan Gambo, alikanusha madai hayo na kudai kuwa wateja wake walikuwa wanajikinga dhidi ya mhasiriwa. Pia, aliomba mahakama kuwapa vifungo vya nje kwa sababu ni wazazi wanaotegemewa.
Licha ya maombi hayo, Hakimu Ongondo alisema kuwa aliangazia mambo hayo lakini kitendo cha watatu hao ni vyema kiadhibiwe kwa kifungo cha ndani.