Bodi ya utalii hapa nchini imewahakikisha wasafiri wa kimataifa kwamba nchi hii ni salama, licha ya ghasia za hivi maajuzi zilizochochewa na kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2024.
Mwenyekiti wa bodi hiyo Francis Gichaba, alisema kuwa wanafahamu wasiwasi ambao huenda ulitokana na ghasia hizo kuhusiana na usafiri hapa nchini, lakini akasema kuwa maeneo na vituo vyote vya kitalii havijaathiriwa na viko wazi kwa wageni.
“Tunawahakikishia wageni wetu kuwa wanaweza zuru maeneo yote ya kitalii hapa nchini,’ alidokeza mwenyekiti huyo.
Gichaba alisema kuwa viwanja vikuu vya ndege nchini, vina kanuni madhubuti za kiusalama na vinatekeleza shughuli zake kikamilifu.
“Viwanja vyote vya ndege hapa nchini vinaendesha shughuli zao kikamilifu, huku ndege zikiwasili na kutua kama kawaida,” alisema Gichaba.
Gichaba aliongeza kuwa usafiri wa barabarani reli uko wazi, ikiwa ni pamoja na reli ya kisasa SGR ambayo inaunganisha Mombasa na Nairobi.
Alisema kuwa bodi hiyo inashirikiana kwa karibu na maafisa kushughulikia wasiwasi wowote na kuhakikisha wageni hawakabiliwi na tatizo lolote.
Mwenyekiti huyo waw bodi pia aliwahakikishia wageni kwamba sekta ya utalii iko imara na imejitolea kuhakikisha wageni wote wanaburudika kikamilifu.