Wataalamu wa lishe kutoa huduma kupitia mtandao

Marion Bosire
1 Min Read

Taasisi ya wataalamu wa lishe “Kenya nutritionists and dieticians institute – KNDI” imeanzisha mpango wa kuweka wataalamu wa fani hiyo wapatao 500 kwenye tovuti yake chini ya mpango wa kutoa huduma kwa umma kupitia mtandao.

Mkurugenzi mtendaji wa KNDI Daktari David Okeyo alisema wataalamu wa lishe watakuwa wanajiunga na wataalamu wengine wa sekta ya afya kwa jumla kutoa huduma zao mtandaoni kwa wanaozihitaji.

Akizungumza wakati wa hafla ya 9 ya kutoa leseni za kuhudumu kwa wataalamu wa lishe 1200 waliohitimu Daktari Okeyo alisema kwamba wanaohitaji huduma za mawaidha ya lishe wanaweza kuunganishwa na wahudumu hao kupitia mtandao.

Alisema teknolojia imerahisisha mtagusano wa wataalamu na wateja wao kupitia mtandao ambapo wanapokea huduma.

Mwanachama wa baraza la taasisi ya KNDI Profesa Gordon Nguka kwa upande wake alitoa changamoto kwa wataalamu waliopokea leseni za kuhudumu kuhakikisha wanatoa huduma kwa wakenya bila ubaguzi.

Wataalamu waliopokea vyeti nao walidhihirisha kujitolea kwa kazi yao baada ya kukamilisha mpango wa uanagenzi wa muda wa miaka miwili.

Share This Article