Maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Mugutha kwa ushirikiano na maafisa wa serikali ya taifa, wamewatia nguvuni washukiwa wawili wa ulanguzi wa mihadarati katika eneo la Kimbo kaunti ya Kiambu.
Idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI, ilisema wawili hao Tyson Mwai mwenye umri wa miaka 30 na Samson Gathuki mwenye umri wa miaka 21, walikamatwa wakati wa operesheni wakiwa na vipande 800 vya bangi.
“Maafisa hao hawakupata tu bangi, lakini pia walipata mifuko 13 ya plastiki ikiwa na bangi ya gramu 35 kila moja, mifko tano ya plastiki ikiwa na gramu 130 kila moja, mifuko 44 ikiwa na gramu 16 kila moja na mashini mbili za kupima uzani,” ilisema idara ya DCI.
Kwa sasa wawili hao wanazuiliwa na polisi, kabla ya kufikishwa mahakamani.
Kwingineko maafisa wa polisi Moyale walikuwa wakishika doria, walinasa kilo 100 za bangi zilizokuwa zikisafirishwa kwa pikipiki.
Maafisa hao walimsimamisha mwendeshaji wa pikipiki yenye nambari za usajili KMGM 369D,lakini alishuka na kutoroka huku akiliwacha pikipiki na bangi hiyo nyuma.
Bangi na pikipiki hiyo zinazuiliwa na polisi.