Washukiwa wawili wa ulaghai wamekamatwa na makachero kwa kupokea fedha kutoka kwa raia kwa kisingizo kuwa watawasaidia kupata kazi.
Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI inasema David Thuo Njehia na Kyalo Kilonzo walikamatwa kwenye barabara ya Ngong baada ya kuwalaghai raia wasiokuwa na habari zaidi ya shilingi 880,000.
Washukiwa walisingizia kuwa wafanyakazi wa kampuni ya kutoa huduma za maji na taka ya Nairobi.
“Wawili hao wamekuwa wakitumia mahangaiko ya Wakenya wanaotafuta ajira kujinufaisha kwa kuwaahidi kuwatafutia ajira katika mashirika ya serikali,” inasema DCI katika taarifa.
Makachero waliwakamata wakati walikuwa wamepokea shilingi 100,000 zaidi kutoka kwa mtu aliyetafuta ajira aliyekuwa ameahidiwa kazi ya kudumu katika kampuni ya kutoa huduma za maji na taka ya Nairobi.
Walipohojiwa, ilibainika kuwa washukiwa hao wawili wana mazoea ya ulaghai na wamekuwa wakisakwa na makachero katika eneo la Dandora.