Maafisa wa idara ya upelelezi wa jinai DCI, wamesambaratisha kundi la wezi wa pikipiki ambalo limekuwa likitekeleza wizi huo kati ya Kenya na nchi moja jirani.
Kulingana na maafisa hao, kundi moja la majambazi limekuwa likiiba pikipiki kutoka miji mbalimbali nchini Kenya na kuzisafirisha hadi mjini Loitoktok ambako zinaingizwa kisiri katika nchi moja jirani.
Mshukiwa mmoja, Agnes Wambui, anayeaminika kutumiwa kuwavutia waendeshaji pikipiki wamsafirishe kabla ya pikipiki zao kuibwa, ndiye aliyekuwa wa kwanza kukamatwa na makachero.
Maafisa hao wamesema yeye husingizia kuwa abiria na kuwahadaa waathiriwa wake wakiwa njiani kabla ya kutoweka na pikipiki zao.
“Huku akijisingizia kuwa abiria, Wambui huwapumbaza waathiriwa kabla ya kutoweka na pikipiki zao,” ilisema DCI.
Mshukiwa huyo aliwaelekeza maafisa wa upelelezi hadi walikokuwa wenzake Daniel Mwaniki na William Nkadanyo anayefahamika kwa jina lingine kama Saningo.
Nkadanyo alikamatwa mjini Loitoktok ambako anaaminika kuwa na soko tayari la pikipiki za kuibwa.
Maafisa hao pia walipata pikipiki na rununu zinazoaminika kuibwa kutoka Juja, kaunti ya Kiambu.
Washukiwa hao wanakabiliwa na kesi za uhalifu katika maeneo ya Ongata Rongai, kaunti ya Kajiado na Diani, kaunti ya Kwale.
Tembe 30 zinazoaminika kuwa za kuwapumbaza watu zilipatikana kutoka kwa washukiwa hao.