Washukiwa watatu wa ulaghai wa dhahabu ghushi wakamatwa

Marion Bosire
4 Min Read

Washukiwa watatu wamekamatwa na maafisa wa upelelezi wa jinai nchini DCI kufuatia kuhusika kwao na ulaghai wa shilingi milioni 340 walizopora raia wawili wa kigeni katika mpango unaohusu dhahabu gushi.

Ulaghai huo ulianza Juni, 2022 wakati wanabiashara wenza Marco Colombo Conti na Satbinder Singh walikuja Kenya kununua kilo 100 za dhahabu kutoka kwa Allain Mwadia Nvita.

Marco alilipa ushuru wa dola laki 4 za Marekani na makato mengine kwa kampuni ya wanasheria iitwayo Squire AfriLaw Consult Limited.

Muuzaji aliahidi kumpa kilo 12 za dhahabu kama zawadi ambayo angebeba kwenye mkoba wa mkononi anaposafiri akauze ili arejeshe pesa alizolipa kama ushuru.

Muuzaji huyo hata hivyo alibadili msimamo akisema zawadi hiyo ingejumuishwa kwenye mzigo mkubwa wa dhahabu ambao sasa ungekuwa kilo 112.

Mzigo huo akaambiwa ungewekwa kwenye makasha ya Mysafe Vaults huko Village Market eneo la Gigiri kaunti ya Nairobi.

Marco aliondoka Kenya akarejea Februari 5, 2024 akiwa na Satbinder Singh aliyetaka kununua dhahabu hiyo.

Satbinder alitambulishwa kwa muuzaji wa dhahabu hiyo Allain Mwadia Nvita, Lehman John Raymond na Daniel Ogot wa kampuni ya Patvad Trading Co. Ltd na Frank Kateti raia wa Tanzania.

Kwa mara nyingine, Allain aliwaahidi kilo 31 za dhahabu kama zawadi ambayo wangebeba kwenye mikoba yao kurejesha pesa ambazo Marco alitumia awali kulipa ushuru na gharama kusafirisha kilo 112 za dhahabu iliyokuwa imewekwa.

Walaghai hao kisha wakaitisha Satbinder na kampuni ya Asianic Limited Euro elfu 162,240 na Euro elfu 548,830 mtawalia.

Baadaye tena Asianic ikaitishwa Euro 14,112 za kulipia usafirishaji wa kilo 112 za dhahabu, malipo yote yakifanywa Februari 8, 2024.

Tarehe 9 Februari, 2024, raia hao wa kigeni walikwenda kuchukua zawadi ya kilo 31 za dhahabu kutoka kwa makasha ya Mysafe Vaults wakaenda kwa afisi ya Daniel Ogot wakala wa usafirishaji wa mizigo nje.

Kasha hilo lilifunguliwa wakagawa dhahabu hiyo katika sehemu mbili ikawekwa kwenye masanduku mawili ya chuma yaliyofungwa na kuwekewa vibandiko vyote hitajika.

Wakielekea uwanja wa ndege waliahidiwa kwamba watabebewa mizigo hiyo hadi huko na Daniel Ogot na Frank Kateti lakini wakakosa kuifikisha huko.

Raia hao wa kigeni hawakuwa na cha kufanya ila kuabiri ndege na kuondoka. Wakiwa Italia Ogot akawaambia kwamba kulitokea shida katika uzani waliokuwa wameandika na uzani halisi wa mizigo hiyo na dhahabu hiyo ikachukuliwa na maafisa husika katika uwanja wa ndege.

Ogot aliwahadaa kwamba kampuni yake inatozwa faini ya asilimia 20 ya thamani ya mizigo hiyo sawa na dola 1,562,000 na iwapo hangelipa, mizigo hiyo ingetwaliwa na serikali kabisa.

Satbinder alilazimika kurejea Kenya akalipa Euro 1,438,460 ambazo aliweka kwenye akaunti ya walaghai hao bila kujua alikuwa akitapeliwa.

Alirejea Uingereza Machi 20, 2024 bila dhahabu hiyo huku washirika wake nchini Kenya wakiendelea kumhadaa.

Alimwandikia barua kamishna mkuu wa shirika la kukusanya ushuru nchini KRA kutafuta kujua uhalali wa stakabadhi alizopatiwa na suala hilo likakabidhiwa DCI.

Uchunguzi umebainisha kwamba stakabadhi hizo ni ghushi na wahusika hawakuwa wafanyakazi wa KRA walivyojisingizia, kampuni ya Patvad Trading Limited haina leseni ya wizara ya madini na kampuni ya ndege ikakana kutoa tiketi walizokuwa nazo.

Watu hao walilaghaiwa jumla ya Euro milioni 2,168,258.91 sawa na shilingi milioni 341,949,292 za Kenya.

Share This Article