Washukiwa watatu mahakamani kwa kutapeli raia wa kigeni

Marion Bosire
2 Min Read

Washukiwa watatu ambao ni Abdul Razak Rehan, Mohammed Amin Suleiman na Ebrahim Ahmed Ebrahim wamefikishwa katika mahakama ya Milimani leo kwa kosa la kubuni mpango waliotumia kulaghai raia wa Pakistan zaidi ya shilingi milioni 116.

Watatu hao walijisingizia kuwa wenye ujuzi wa biashara ya vyuma kuu kuu na betri za magari na wakavutia mwekezaji huyo akaja Kenya huko wakimahidi biashara ya kufana katika sekta hiyo.

Ebrahim Ahmed Ebrahim alimshauri jamaa huyo asajili kampuni, hatua ambayo alimdanganya inagharimu shilingi milioni 7. Mohammed Amin Suleiman na Abdul Rian Shul walijisingizia kuwa mwekahazina wa afisi ya kusajili kampuni nchini na msaidizi wa kibinafsi wa Naibu Rais mtawalia kisha wakapokea pesa hizo.

Mwekezaji huyo alihadaiwa pia akatoa fedha zaidi ambazo alidanganywa ni ada ya ghala la kuweka bidhaa, za kununua vyuma kuu kuu na betri za magari, ushuru na vibali na kwa jumla wakamwibia shilingi milioni 116.

Uchunguzi uliotekelezwa na maafisa wa upelelezi DCI uligundua kwamba stakabadhi zote walizompa mwekezaji huyo zilighushiwa.

Maafisa walianza kusaka washukiwa hao na kufanikiwa kuwapata kwenye maficho yao na leo wakafikishwa mahakamani Milimani. Walikana mashtaka yote dhidi yao na kuachiliwa kwa bondi ya shilingi milioni 5 na mdhamini wa kiasi sawa.

Kesi hiyo itatajwa Septemba 9, 2024.

Share This Article