Washukiwa watano wa wizi wakamatwa Nairobi

Tom Mathinji
2 Min Read
Washukiwa wa wizi wakamatwa na makachero wa DCI Jijini Nairobi.

Maafisa wa upelelezi wa maswala ya jinai DCI, wamewakamata washukiwa watano kuhusiana na wizi wa shilingi 900,000 pamoja na dola 15,000 za Marekani kutoka kwa mfanyabiashara mmoja anayehudumu katika mtaa wa South C jijini Nairobi, wiki mbili zilizopita.

Kupitia mtandao wa X, idara ya DCI ilisema watano hao walitiwa nguvuni baada ya msako mkali kutekelezwa, kwa lengo la kukomesha wizi wa magari Jijini Nairobi.

Kulingana na DCI, mwathiriwa wa wizi huo aliyepiga ripoti katika kituo cha polisi cha Akila  mtaani Langa’ata, aliegesha gari lake katika kituo kimoja cha kuuza petroli, ambapo aliingia katika duka la kuuza vipuri vya magari, lakini aliporejea kwenye gari lake alipata dirisha la nyuma limevunjwa na mkoba wake uliokuwa na kadi kadhaa za benki umeibwa.

Kulingana na taarifa hiyo ya polisi, mwathiriwa huyo alipokea ujumbe mfupi ukiashiria kuwa shilingi 40,000 zimetolewa katika akaunti yake ya benki ya KCB, na shilingi zingine 40,000 zimetolewa katika akaunti yake ya benki ya DTB.

Polisi walianzisha msako na kuwakamata washukiwa hao ambao ni pamoja na Charles Nzomo, Paul Mukungi, Vincent Juma Raguma, Jane Mueni Mutinda na Shaban Rashid Maingi.

Wanazuiliwa na maafisa wa upelelezi wa DCI katika kipindi hiki cha sherehe za sikukuu ya Pasaka.

Maafisa hao wanamtafuta mshukiwa wa sita Rodgers Ndung’u ambaye anaaminika kuwa ametorokea Jijini Mombasa.

Makachero hao wanaamini kwamba genge hilo lina uhusiano na washukiwa 4 waliokamatwa mnamo mwezi Februari mwaka uliopita baada ya msururu wa matukio ya kuvunja magari wakitumia vifaa  vya ujambazi sawa na vilivyonaswa mtaani South C jijini Nairobi.

TAGGED:
Share This Article