Afisa wa polisi ni miongoni mwa washukiwa watano waliokamatwa kwa kujisingizia kuwa maafisa wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi, EACC.
Watano hao wanaaminika kuwa sehemu ya genge ambalo huwahangaisha wananchi katika kaunti ya Kitui, kwa kufanya operesheni haramu wakijisingizia kuwa maafisa wa EACC.
Washukiwa hao walikamatwa Ijumaa, walipokuwa wakiendesha operesheni haramu katika afisi za serikali ya kaunti ya Kitui.
Kwenye taarifa leo Jumamosi, tume ya kukabiliana na ufisadi hapa nchini EACC, ilisema washukiwa hao walikuwa wamevamia makao ya Mkurugenzi wa mapato wa serikali ya kaunti ya Kitui, wakidai wanachunguza ufujaji wa fedha.
Tume hiyo ilipokea habari kutoka kwa afisa mkuu wa polisi wa eneo hilo, akithibitisha kuwa watu hao sio maafisa kutoka tume ya EACC.
Washukiwa hao waliokamatwa wakiendesha gari aina ya Toyota Fielder lenye nambari za usajili KDC 846X, ni pamoja na:
- CPL Anne Mutheu, mwenye umri wa miaka 46, ambaye ni afisa wa polisi katika kituo cha polisi cha Muthangari.
- Sheddy Kakai,mwenye umri wa miaka 37
- Permelus Kasama, mwenye umri wa miaka 48
- Joseph Musembi, mwenye umri wa miaka 34
- David Bembe, mwenye umri wa miaka 33.
Kwa sasa washukiwa hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha kitui, huku uchunguzi zaidi ukiendelea.