Washukiwa wa wizi wa simu wakamatwa Nairobi

Tom Mathinji
2 Min Read

Washukiwa wanne wanaohusishwa na msururu wa visa vya wizi wa simu za rununu jijni Nairobi, walikamatwa na maafisa wa polisi siku ya Ijumaa.

Malumasi Aisha na Agaba Anestus Majuni ambao ni raia wa Uganda walikamatwa pamoja na Sarah Njeri na dadake Mary Wangui kwenye operesheni iliyotokana na habari za kijasusi iliyotekelezwa na maofisa wa idara ya ipelelezi wa jinai katika sehemu ya katikati mwa jiji.

Malumasi aliyekuwa wa kwanza kuitiwa nguvuni, alipatikana na kifurushi kilichokuwa na simu za rununu za kisasa 13, zilizodhamiriwa kuuzwa kimagendo nchini Uganda.

Baada ya kukamatwa aliwapelekea maafisa hao katika duka moja E17 katika kituo cha biashara cha Munyu, ambako washirika wake Sarah Wangari na Mary Wangui walifumaniwa wakipokea simu zaidi za wizi.

Watatu hao waliwaelekeza maafisa wa upelelezi kwa mshukiwa wa nne Agaba Majuni, ambaye alikuwa akisubiri kukabidhiwa shehena ya simu hizo katika kituo cha mabasi ya Simba Coach. Washukiwa hao watashtakiwa kwa kosa la wizi.

Idara ya DCI ilisema imepanua wigo wake wa ili kuwatia nguvuni washukiwa zaidi, katika kile kinachoaminika kuwa biashara ya kuingiza kimagendo bidhaa zilizoibwa nchini Uganda.

“Wezi wa simu za rununu wanakuwa na wakati mgumu kuendeleza biashara yao haramu kutokana na utumizi wa kisasa wa teknolojia na maafisa wa DCI,” ilisema DCI kupitia kwa taarifa.

TAGGED:
Share This Article