Watu wanne ambao wanashukiwa kuhusika katika wizi wa shilingi milioni 94 za kampuni ya maduka ya jumla Quikmart zilizokuwa zikipelekwa benki wamekamatwa.
Kulingana na maafisa wa polisi, washukiwa hao wanne walipatikana katika sehemu za Rongai, Kayole na barabara ya Thika Jumamosi na milioni 9.1 zilipatikana.
Gari ambayo washukiwa hao walitumia kukwepa na pesa hizo ilitambuliwa kupitia kamera za CCTV na ikafuatiliwa.
Polisi wanasema mmoja wa washukiwa ambaye ni mmiliki wa gari hilo alikamatwa wa kwanza huko Rongai akijaribu kuibadilisha ili isitambulike kwa urahisi.
Yeye ndiye aliongoza maafisa wa polisi hadi walikokuwa washukiwa wengine na katika nyumba ya mmoja wao huko Kasarani ndiko milioni 9.1 zilipatikana.
Awali polisi walipata kasha lililokuwa limebeba pesa hizo mtaani Karen na wanaamini hapo ndipo washukiwa waligawana hizo pesa.
Kampuni ya Quickmart kwenye taarifa ilithibitisha kwamba pesa hizo zilikuwa zimetoweka lakini ikafafanua kwamba wakati wa kutoweka zilikuwa mikononi mwa kampuni ya Wells Fargo ambako washukiwa walikuwa wanafanya kazi.
Awali idara ya upelelezi wa jinai DCI ilikuwa imetoa picha za washukiwa wawili waliotambuliwa kama Daniel Mungai aliyekuwa kamanda wa kikosi kidogo kilichojukumiwa kusafirisha pesa hizo na dereva Anthony Nduiki walitoweka asubuhi ya Novemba 6 wakitumia gari aina ya Isuzu canter nambari ya usajili KBA 517T.
Inasemekana kwamba walikwenda kuchukua pesa hizo kama kawaida lakini wakatoweka bila ulinzi kutoka kwa maafisa wa polisi kama ilivyo ada.
Polisi wa kitengo cha AP ambao walistahili kuandamana na wawili hao waliwasubiri lakini hawakutokea ndiposa wakafahamisha kampuni ya Wells Fargo.