Washukiwa wawili wa wizi wa kimabavu ambao wamekuwa mafichoni kwa muda wa miezi miwili, wametiwa nguvuni.
Washukiwa hao wanadaiwa kumshambulia dereva wa lori katika soko la Askote lililoko kaunti ya Vihiga, aliposimama kununua bidhaa.
Philip Kitwa na Kennedy Arunga walikamatwa wakiwa katika eneo la Emuhaya, kaunti ya Vihiga baada ya uchunguzi wa kitaalam kutoka maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai wa eneo la Magharibi mwa nchi.
Katika tukio hilo la tarehe 30 mwezi Agosti mwaka 2023, dereva huyo alivamiwa na washukiwa hao waliokuwa wamejificha katika shamba la mahindi, aliposimama kununua bidhaa katika soko la Askote.
Mwathiriwa huyo alipata majeraha mabaya ya panga na rungu kutoka kwa majangili hao, kabla ya kupelekwa katika hospitali ya Equator iliyoko eneo la Luanda na msamaria mwema.
Wezi hao wanazuiliwa katika korokoro za polisi, wakisubiri kufikishwa mahakamani siku ya Jumatatu.