Washukiwa wa uwindaji haramu wakamatwa Homa Bay, pembe ya kifaru ya mamilioni ya pesa yanaswa

Martin Mwanje
1 Min Read
Washukiwa wa uwindaji haramu waliokamatwa Homa Bay

Wapelelezi na maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Homa Bay wamefanikiwa kuwakamata washukiwa watatu wa uwindaji haramu na kunasa pembe ya kifaru ambayo thamani yake inakadiriwa kuwa shilingi milioni 2.9. 

Kwa kushirikiana na maafisa wa Shirika la Wanyama Pori nchini, KWS kutoka Mbuga ya Kitaifa ya Ruma, maafisa hao waliwakamata watatu hao kwenye soko la Rodi katika kaunti ndogo ya Homa Bay baada ya kupokea taarifa za kijasusi.

Washukiwa hao ni Bernard Omondi Sunga ambaye ni mwanajeshi wa Vikosi vya Ulinzi nchini, KDF na wandani wake George Oloo na Argwings Watta.

Walipatikana wakiwa kwenye gari jeusi ambalo nambari yake ya usajili ni KBM 463G.

Lilipopekuliwa, ilibainika kuwa pembe ya kifaru yenye uzito wa kilo 2.9 ilikuwa imefichwa kwenye gari hilo.

Washukiwa hao watatu wamefikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka.

Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI inasema imedhamiria kushirikiana na washikadau mbalimbali kuangamiza jinamizi la uwindaji haramu wa wanyama pori nchini.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *