Washukiwa wa ulanguzi wa bangi wanaswa Nakuru

Tom Mathinji
1 Min Read
Polisi wanasa bangi katika kaunti ya Nakuru.

Washukiwa watatu wamekamatwa wakisafirisha bangi, waliyoisingizia kuwa chakula cha mifugo katika kaunti ya Nakuru.

walikamatwa na maafisa wa kushughulikia makosa ya jinai DCI, baada ya kupashwa habari kuhusu gari iliyotiliwa shaka. Maafisa hao walizuia gari hilo katika eneo la Subukia likielekea mjini Nakuru.

Katika operesheni hiyo iliyotekelezwa jana Ijumaa, bangi ya kilo 138 ilipatikana ndani ya gari KBX 684H na pia katika gari aina ya Toyota Crown KBZ 861H.

“Baada ya kupatikana kwa bangi katika gari hiyo, dereva Evans Oluoch Rogo mwenye umri wa miaka 32, aliwapeleka maafisa wa polisi walikokuwa washirika wake wawili, waliopatikana wakijivinjari katika hoteli ya Qualit,” ilisema DCI kupitia ukurasa wa X.

Ali Abdikadir Ali mwenye umri wa miaka 30 na Ortofa Dida mwenye umri wa miaka  28, pia walikamatwa wakiwa na bangi yenye uzani wa kilo 79.

Kitengo cha kukabiliana na mihadarati, kimeweka mikakati dhabiti ya kukabiliana na ulanguzi wa mihadarati katika lengo la kukomesha kabisa biashara hiyo haramu.

TAGGED:
Share This Article