Washukiwa wa ulaghai wa usajili wa magari wakamatwa

Marion Bosire
2 Min Read

Washukiwa 11 wamekamatwa na wapelelezi kuhusiana na ulaghai wa kiwango cha juu wa usajili wa magari katika mamlaka ya kitaifa ya usafiri na usalama barabarani NTSA.

Hii ni baada ya wapelelezi kutekeleza ukaguzi wa kina wa mfumo jumuishi wa usimamizi wa usafiri wa mamlaka hiyo ya kitaifa ya usafiri na usalama barabarani – TIMS baada ya kushuku kwamba watendakazi wafisadi wa NTSA walikuwa wakiendesha akaunti haramu za kusajili magari.

Mshukiwa mkuu Jimmy Kibet Wayans, alikamatwa katika nyumba moja mtaani Lavington ambapo alikuwa akiendesha akaunti tatanishi ambayo imeingilia mfumo wa TIMS kusajili magari kwa njia haramu.

Kati ya miezi ya Machi hadi Aprili pekee, nambari za chasis za magari 47 zilibadilishwa huku nyingine 54 zikiongeza kiharamu kwenye mfumo huo ishara ya ulaghai wa kiwango cha juu unaotekelezwa na wahalifi hao.

Uchunguzi ulibainisha pia kwamba mshukiwa ambaye sio mfanyikazi wa NTSA alikuwa na majukumu makubwa haramu na amekuwa akidhibiti akaunti nyingi za uwongo kwenye mfumo wa NTSA.

Wapelelezi wanachunguza pia namna akaunti ambayo ilifungwa ya afisa wa teknolojia ya mawasiliano wa NTSA ilifunguliwa tena na ilikuwa ikitumika kwa shughuli haramu hata baada yake kujiuzulu, Julai, 2022.

Watendakazi watatu wa NTSA Anthony Waithaka, David Migwi na David Kimaren pia walikamatwa kuhusiana na uhalifu unaohusisha watendakazi wa mamlaka ya kukusanya ushuru nchini KRA.

Mshukiwa mmoja kutoka KRA Boniface Njoroge amekamatwa, wapelelezi wanapojitahidi kuhakikisha wanashtaki washukiwa hao ambao wamesababisha serikali ipoteze pesa nyingi.

Share This Article