Washukiwa wanne wanaohusishwa na mlipuko wa gesi eneo la Embakasi uliotokea juma lililopita ambapo hadi kufikia sasa watu saba wamefariki, watazuiliwa kwa muda wa siku 21 ili kutoa fursa kwa maafisa wa polisi kukamilisha uchunguzi.
Washukiwa hao ni pamoja na mmiliki wa kituo hicho cha gesi Derrick Kimathi, Joseph Makau, David Walunya Ong’are na Marrian Mutete Kioko ambao ni maafisa wa shirika la taifa linalosimamia mazingira (NEMA).
Hakimu anayeskiliza kesi hiyo Dolphina Alego alikubaliana na upande wa mashtaka kwamba suala hilo linahusiana na maslahi ya umma na maafisa wa upelelezi wanahitaji muda zaidi kufanya uchunguzi wa kina.
Upande wa mashtaka uliiambia mahakama kuwa watu hao wanne walikuwa wamejificha tangu kuripotiwa kwa kesi hiyo na rasilimali nyingi zimetumika kuwasaka, na kuongeza kuwa hawapaswi kuachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu.
Wanne hao wanachunguzwa kuhusiana na mauaji, utepetevu na utumizi mbaya wa mamlaka.
Takriban watu sita walifariki na wengine 300 kujeruhiwa katika mkasa huo uliotokea wiki jana.
Kesi hiyo itatajwa tarehe Februari 28, 2024.