Washukiwa wa mauaji ya Albert Ojwang wanyimwa dhamana

Marion Bosire
1 Min Read
Marehemu Albert Ojwang

Aliyekuwa afisa msimamizi wa kituo cha polisi cha Central Samson Kiprotich Talaam na washtakiwa wenza katika kesi ya mauaji ya Albert Ojwang, wamepata pigo baada ya mahakama kuu kuwanyima dhamana.

Jaji wa mahakama ya Kibera Diana Kavedza katika uamuzi wake alisema washtakiwa hao sita watasalia kizuizini hadi pale ambapo mashahidi wakuu watakapomaliza kutoa ushahidi wao.

Mahakama ilipata kwamba kuna tishio kubwa la kuingiliwa kwa mashahidi hao wakuu, hasa wale wanaohudumu katika huduma ya taifa ya polisi.

Sasa kikao cha maandalizi ya kesi ya mauaji ya Albert Ojwang kitaanza Novemba 17 hadi 21,2025.

Upande wa utetezi uliagizwa kuchagua tarehe ya kusikilizwa mahakamani kati ya Januari 26 na 30 2026, na kisha kuandikia mahakama nyaraka za kudhibitisha upatikanaji wao.

Jaji Kavedza alisema kwamba kesi kama hizi ambazo huvutia hisia za umma zinafaa kupatiwa kipaumbele, ndiposa ameamua kwamba atatangaza tarehe ya kuisikiliza ifikapo Januari, 2026.

Katika maelekezo yake na jinsi ya kushughulikia kesi hiyo, Jaji huyo alisema kwamba mashahidi wawili wakuu watafichwa na sauti zao kubadilishwa.

Katika kuchagua tarehe za kusikilizwa, wahusika walielekezwa kwamba ni mashahidi wanne watakaosikilizwa kwa wakati mmoja huku kukiwa na mashahidi 18 wa upande wa mashtaka.

Website |  + posts
Share This Article