Maafisa wa polisi wamewakamata washukiwa watatu wanaohusishwa na mauaji ya afisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka(IEBC) kaunti ya Kilifi Aisha Abubakar.
Watatu hao Isa Omari, Brian Shikuku Mudari na Bryan Templer Oyare, walikamatwa kutoka maficho yao sehemu tofauti katika eneo la Pwani siku ya Jumatatu, kufuatia operesheni iliyochukua muda wa siku saba.
Kulingana na idara ya uchunguzi wa makosa ya jinai DCI, washukiwa hao pia walinaswa na bidhaa zinazoshukiwa kuwa ziliibwa kutoka nyumbani kwa Abubakar.
Idara hiyo ilisema washukiwa hao walimdunga kisu mara kadhaa mwathiriwa na kumuua kabla ya kutoroka na simu zake mbili aina ya Samsung, runinga ya inchi 65, vinanda, kadi za ATM ambazo waliitisha nambari za siri, miongoni mwa bidhaa zingine.
“Uchunguzi wa kisayansi umesababisha kutiwa nguvuni kwa washukiwa hao, ambapo pia simu ya mwanawe wa kiume wa mwathiriwa pamoja na bidhaa zingine zilipatikana,” ilisema DCI kupitia ukurasa wake wa X.
Idara hiyo ilisema wahalifu hao waliingia nyumbani kwa marehemu kupitia dirishani.
“Tunaendelea kufanya uchunguzi,” iliongeza idara hiyo.