Wasanii kuwasilisha malalamiko ya mrabaha kwa mashirika ya serikali

Alphas Lagat
2 Min Read

Wasanii kutoka pembe zote za nchi wanapanga mkutano jijini Nairobi siku ya Jumanne, Machi 5, kwa minajili ya kuwasilisha malalamiko yao kuhusu ulipaji wa mrabaha kwa mashirika ya serikali.

Wasanii hao watakongamana katika jumba la Pioneer lililoko katika barabara ya Moi kuanzia saa tatu asubuhi ambapo wanatarajiwa kuwasilisha malalamiko yao na kutetea haki zao.

Mwenyekiti wa muungano wa wasanii (MAAK) Justus Ngemu, alisema kuwa maandamano ambayo yanatumia alama za reli #ArtistsDemo na #PesaKwaMsanii yanalenga kukabiliana na changamoto zinazokumba wasanii.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Ngemu alisema kuwa wasanii wanataka kuungwa mkono na Bunge la Taifa, Seneti, Jaji Mkuu na Waziri anayehusika na sanaa ili kuwaelekeza kuhusu changamoto za kifedha ambazo wasanii wanapitia.

“Wasanii wanatafuta kutambuliwa kwa mchango wao katika Pato la Taifa la Kenya na mandhari ya kitamaduni na wanatoa wito wa kuchukuliwa hatua za kuimarisha na kuwezesha jamii ya wasanii,” alisema Ngemu.

Alitaja ulinzi wa hakimiliki, mizozo ya hivi majuzi kati ya wasanii na mashirika ya usimamizi wa pamoja na madai ya utumiaji mbaya wa mirabaha iliyokusudiwa kwa wasanii na ukosoaji uliotolewa dhidi ya Halmashauri ya Hakimiliki ya Muziki ya Kenya kwa ukosefu wake wa uwazi na uwajibikaji, kama baadhi ya masuala ya msingi ambayo wanataka kushughulikiwa katika maombi hayo.

Alphas Lagat
+ posts
Share This Article