Waraibu 60 wa mihadarati katika kaunti ya Mombasa, wameokolewa na kupelekwa katika vituo vya kurekebishia tabia vilivyoko kaunti ya Kwale.
Mkewe naibu Rais mchungaji Dorcas Rigathi, siku ya Ijumaa alitimiza ahadi zake alizotoa kwa familia zinazoishi mitaani katika maeneo ambapo mihadarati hutumiwa kaunti ya Mombasa.
Waraibu hao ambao wameazimia kurekebisha tabia, walikuwa watumizi wa dawa za kulevya aina ya cocaine, heroin, nicotine, miraa na pombe miongoni mwa mihadarati mingine.
Waraibu hao waliaga familia zao huku wakielekea katika vituo hivyo vya kurekebishia tabia, watakakoishi kwa muda wa miezi mitatu ijayo.
Alipowatembelea, mchungaji Dorcas aliwapelekea bidhaa za kimsingi kama vile sabuni, viatu na dawa ya meno, huku akiwahimiza kuwa wavumilivu wakati wa kipindi hicho cha kurekebishwa tabia.
“Maisha ya mtoto mmoja ni muhimu. Nilipowatembelea walinieleza kuwa watu wengi waliwapa ahadi kuwa watawasaidia. Hawakuniamini niliposema nitawaletea chakula. Lakini siku hiyo hiyo niliwaletea chakula. Siku ya pili niliwapelekea kambi ya matibabu bila malipo na sasa wengine wako katika vituo vya kurekebisha tabia,” alisema mchungaji Dorcas.
Aidha Dorcas alitoa wito kwa wafadhili zaidi katika sekta ya umma na ile ya kibinafsi kujitokeza ili kushughulikia idadi kubwa ya wale wanaotaka kurekebishwa tabia.