Wapiganaji wa Houthi washambulia ndege ya mizigo ya Marekani

Tom Mathinji
2 Min Read

Waasi wa Houthi wameipiga meli ya mizigo inayomilikiwa na Marekani kwa kombora la balestiki katika pwani ya Yemen, Marekani inasema.

Maafisa wa meli hiyo, Gibraltar Eagle, waliripoti kuwa “hakuna majeraha au uharibifu mkubwa”, kulingana na kamandi ya jeshi la Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati (Centcom).

Meli hiyo yenye bendera ya Visiwa vya Marshall inaendelea na safari katika Ghuba ya Aden.

Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran wamekuwa wakishambulia meli tangu Novemba, kupinga vita vya Israel dhidi ya Hamas.

Kampuni ya usafirishaji ya Eagle Bulk Shipping ilisema kuwa shehena hiyo kubwa ilikuwa imebeba bidhaa za chuma na ilikuwa umbali wa takriban kilomita 160 (maili 100) nje ya pwani katika Ghuba ya Aden ilipopigwa na kombora.

Ilisema meli hiyo “ilipata uharibifu mdogo kwenye sehemu ya kubebea mizigo lakini iko imara na inaelekea nje ya eneo hilo”.

Saa kadhaa kabla ya shambulio hilo Centcom ilisema kuwa kombora jingine lililorushwa kuelekea upande wa Marekani katika Bahari ya Shamu lilinaswa na kuangushwa na ndege ya kivita ya Marekani.

Wahouthi wamekuwa wakishambulia meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu ambazo kundi hilo linasema kuwa zina uhusiano na Israel, au kuelekea kwenye bandari za Israel.

Inasema mashambulizi hayo yanaonyesha lengo lao la kuwaunga mkono Wapalestina na Hamas katika vita vinavyoendelea Gaza, huku Israel ikiendelea na harakati zake za kijeshi huko.

Share This Article