Wapangaji wote wa jengo lililoporomoka katika mtaa wa Uthiru kaunti ya Nairobi wako salama, hayo ni kulingana na afisa anayesimamia majanga katika serikali ya kaunti ya Nairobi, Bramwel Simiyu.
“Wapangaji wote 34 katika jengo lililoporomoka Jumanne usiku wako salama. Awali watu wanne hawakujulikana waliko, lakini wamepatikana,” alisema Simiyu.
Jengo hilo la orofa tano liliporomoka Jumanne usiku na kusababisha operesheni kubwa ya uokoaji, iliyoongozwa na maafisa wa serikali ya kaunti ya Nairobi, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya na wananchi.
Kulingana na Simuyu Jengo lilikuwa likizama polepole, na wakaazi wote waliweza kuruka na kufanikiwa kutoka nje ya jengo hilo.
Alidokeza kuwa maafisa wa maafisa wa dharura wa serikali ya kaunti ya Nairobi wamezingira eneo hilo, wakisubiri usaidizi kutoka kwa maafisa wa vikosi vya ulinzi kutoka kambi ya Kahawa, wanaotarajiwa kuwasili na mbwa wa kunusa kuhakikisha hakuwa watu walionaswa na vifursi vya jengo hilo.
Aidha, afisa huyo alisema serikali ya kaunti hiyo inatoa msaada wa kibinadamu kwa waathiriwa.