Kama njia ya kumkumbuka marehemu mamake, mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi ameandaa sikukuu ya Krismasi kwa kina mama zaidi ya 300 katika eneo bunge lake siku ya Jumanne.
Hafla hiyo imeandaliwa katika shule ya upili ya Parklands Arya na iliwashirikisha kina mama kutoka wadi tano za Parklands, Karura, Kangemi, Mountain View na Kitisuru.
Wanyonyi alitoa zawadi za Krismasi kwa kina mama kama kumbukumbu kwa marehemu mamake mzazi Anne Nanyama Wetang’ula, aliyefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu..
Mbunge huyo alikariri kujitolea kuboresha masIahi ya wakongwe katika eneo bunge lake .
“Huu ni wakati mwafaka wa kuwakumbuka watu muhimu ambao wametulea, huenda hamna uwezo wa kujinunulia vyakula vya kusherehekea Krismasi hii ndio maana nimewaalika hapa niwanunulie Krismasi,” alisema Wanyonyi.
Wanyonyi alichukua fursa hiyo pia kutoa changamoto kwa wakongwe kuliombea taifa hususan matatizo yanayowakumba vijana, akiahidi kubuni mazingira bora yatakayowezesha kuwa na uchumi wenye nafasi za kazi.
Amewataka viongozi kutoa kipaumbele kwa utoaji huduma bora kwa wananchi.
“Katika kila uchaguzi tunawachagua viongozi sita, lakini mnahitaji uwajibikaji kutoka kwangu kama mbunge wenu. Nawataka pia mhakikishe uwajibikaji kutoka kwa kila kiongozi,”akasema Wanyonyi.
Mbunge huyo alitangaza azima yake ya kuwania Ugavana wa kaunti ya Nairobi mwaka 2027 akiahidi kutoa huduma bora kwa wakazi.
Wanyonyi amekosoa uongozi wa sasa wa kaunti ya Nairobi kwa huduma mbovu na miundombinu duni, akiapa kurekebisha utoaji huduma endapo atachaguliwa .