Taasisi ya utafiti na mafunzo ya wanyama-pori-WRTI, imeanza shughuli ya kuyatambua maeneo ya mbuga na vyanzo vya maji ambavyo huenda vikaathirika kutokana na mvua ya El Nino.
Tayari taasisi hiyo imetambua mbuga ya Amboseli na vyanzo vya vya maji vya Bonde la Ufa kuwa maeneo yalio hatarini.
Kadhalika taasisi hiyo imeonya kuwa huenda kukazuka ongezeko la visa vya mtafaruku baina ya binadamu na wanyama-pori, kutoka mbuga zilizofurika, wakihamia ardhi kavu.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa kongamano la Kisayansi lililoandaliwa mjini Naivasha, Mkurungenzi mkuu wa taasisi hiyo Dakta Patrick Omondi, alisema taasisi hiyo inashirikiana na shirika la huduma kwa wanyama-pori kutafuta mbinu mwafaka za kukabiliana na athari za mvua hiyo.
“Taasisi ya WRTI inashirikiana kwa karibu na shirika la huduma kwa wanyamapori KWS , kubuni mikakati ya kuchukua tahadhari karibu na mbuga, ili kupunguza athari za mvua ya El Nino,” alisema Omondi.
Omondi aliongeza kuwa sekta ya wanyamapori hapa nchini imeanza kuimarika baada ya kuathiriwa na ukame wa muda wa miaka miwili.
Aidha alisema wakati wa kipindi hicho cha ukame, hakuna hata kifaru mmoja aliyeangia, akitaka idadi ya ndovu kuwa 36,000.