Gavana wa kaunti ya Nyandarua Daktari Kiarie Badilisha ametoa onyo kali dhidi ya watu wambao wamenyakua ardhi ya umma baada ya eneo moja chepechepe kunyakuliwa na watu wasiojulikana huko Kinangop.
Akizungumza katika eneo la Karia Ka Ndagi, Kiarie alisema kwamba hakuna ardhi ya umma itanyakuliwa katika kaunti ya Nyandarua iwe katika eneo chepechepe au eneo jingine.
Alisema ardhi ya umma haiwezi kutumiwa na watu binafsi bila ya kufuata taratibu zinazofaa kisheria.
Gavana Badilisha alizungumzia suala hilo baada ya lalama za wananchi walioona mstawishaji binafsi akichimba mitaro ya kuondoa maji katika ardhi hiyo ili aweze kuitumia.
Aliahidi kufuatilia suala hilo ambapo atakutana na viongozi kadhaa wa serikali ya kitaifa kujadili.
Iwapo mtu yeyote atapatikana na hatia, Gavana huyo ameahidi kwamba atachukuliwa hatua za kisheria.