Wanjigi aachiliwa kwa dhamana ya milioni 10

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanabiashara na mwanasiasa Jimi Wanjigi ameachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni 10 baada ya kukamatwa jana Jumatatu na kulala katika korokoro za kituo cha polisi cha Kamukunji.

Alifikishwa katika mahakama za Milimani leo Jumanne, Agosti 20, 2024 ambapo alikabiliwa na mashtaka ya kumiliki bunduki kinyume cha sheria.

Wanjigi alitakiwa kuikabidhi mahakama pasipoti yake akisubiri uamuzi wa kesi hiyo unaopangiwa kutolewa Septemba 12, 2024.

Wanjigi na mshukiwa mwenza watafahamu siku hiyo pia iwapo mashtaka dhidi yao yatatupiliwa mbali au la.

Awali, mawakili wa Wanjigi wakiongozwa na Paul Muite waliitaka mahakama iahirishe shughuli ya kukubali au kukataa mashtaka kwani walikuwa na agizo la mahakama la kuzuia kukamatwa kwake.

Agizo hilo, kulingana na Muite, lilielekeza kwamba Wanjigi aachiliwe mara moja iwapo amekamatwa.

Mawakili hao walidai pia kwamba maafisa wa polisi walifutilia mbali kibali cha kumiliki bunduki cha Wanjigi kwa nia mbaya hata ingawa mahakama kuu iliagiza arejeshewe kibali hicho.

Willis Otieno, mmoja wa mawakili hao, alisema kwamba bodi ya kutoa leseni za kumiliki bunduki ilitwaa kibali cha Wanjigi kwa nia ya kumkamata kwa kosa la kumiliki bunduki bila leseni.

Akizungumza mbele ya Hakimu Susan Shitubi, Otieno alisema kwamba makosa aliyowekewa Wanjigi yalikuwa na kasoro nyingi na kwamba polisi walikiuka maagizo ya mahakama.

Wanjigi alijiwasilisha mwenyewe kwa polisi baada ya wao kumtaka afike katika kituo cha polisi na wakaishia kumkamata.

Mlinzi wake kwa jina Kibe anasemekana kudhulumiwa na maafisa wa polisi akiwa kizuizini.

Share This Article