Wanawake Marsabit kuhusishwa katika usimamizi wa ardhi ya jamii

Bruno Mutunga
4 Min Read
Wanawake na wasichana katika jamii za wafugaji wamekuwa wakinyimwa haki za umiliki wa ardhi

Kwa karne nyingi, wanawake na wasichana katika jamii za wafugaji wamekuwa wakinyimwa haki za umiliki wa ardhi, na hata kutohusishwa kamwe katika vikao vya kujadili mambo muhimu yanayohusu jamii zao.

Wakati wote huo, wametwikwa tu jukumu la kusalia nyumbani wakishughulikia masuala ya watoto, mifugo, kufua nguo na kutayarisha vyakula.

Katika kaunti ya Marsabit, asilimia 80 ya ardhi huwa chini ya umiliki wa jamii, jambo ambalo haliruhusu mwanamke yeyote kuwa na usemi katika masuala ya umiliki wa ardhi hiyo.

Na hata katika familia chache ambazo zimefaulu kusajili ardhi yao chini ya umiliki wa kibinafsi, ni asilimia moja tu ya wanawake hasa wale waliofiwa ambao wameweza kujivunia kuwa na umiliki wa ardhi.

Hata hivyo, vizingiti hivi huenda  vikazikwa katika kaburi la sahau kufuatia hatua mpya iliyochukuliwa na baadhi ya jamii katika kaunti ya Marsabit ili kusajili ardhi yao rasmi.

Jamii ya Warendille wanaoishi katika sehemu za Log logo na Karare wamewachagua baadhi ya wanawake kuwa miongoni mwa wanakamati wa kusimamia shughuli za usajili rasmi wa ardhi ya jamii.

Hatua hiyo inatazamiwa kuleta mageuzi makuu katika usimamizi, uangalizi na utekelezaji wa mashauriano baina ya wanajamii kuhusu jinsi ya kutumia vipande vyao vya ardhi.

Kwa mujibu wa mwanachama mpya wa kamati simamizi ya ardhi katika wadi ya Log logo Fatuma Galoro, hatua hii ya kipekee ni ushindi mkuu kwa jamii ya Rendille katika maeneo hayo ambapo wanawake wanakabiliwa na taasubi za kiume.

Ameapa kutoruhusu wanawake kudhulimiwa tena kwa msingi wa umiliki wa ardhi katika maeneo hayo.

Ameongezea kuwa hatua hiyo pia itawawezesha kudhibiti jinsi wawekezaji wanaingia katika makubaliano ya kuitumia ardhi ya jamii, ili wasipitie mlango wa nyuma kupitia viongozi wa kaunti au wanasiasa bila kuwashirikisha wanajamii.

Aidha, Fatuma amevipongeza vipengele katika Katiba ya mwaka 2010 ambavyo huhakikisha ushiriki wa umma katika umiliki na utumizi wa ardhi ya jamii, ili watoe ushauri na maoni yao  kuhusu miradi ya kutekelezwa katika vipande vyao vya ardhi.

Mwanzilishi wa Shirika la Watu Wafugaji, Margaret Super kwa upande wake amesifia hatua hiyo iliyochukuliwa na jamii ya Warendille ili kusajili ardhi yao kwa mujibu wa Katiba.

Ametaja hatua hiyo kama ushindi mkuu kwa wanawake kwa sababu sheria ya ujumuishaji wa wanawake watano na wanamme kumi katika kamati simamizi ya ardhi ya jamii  ni jambo la kihistoria kwa jamii za wafugaji.

Aidha, kwa mujibu wa afisa wa mawasiliano katika shirika la (Community Land Now) CLAN! linaloshughulika na uhamasishaji wa usajili rasmi wa ardhi ya wafugaji Isaack Asugo, jamii zote tano ambazo tayari zimechukua hatua ya kusajili ardhi yao zimeanza kukumbatia uongozi wa wanawake katika masuala ya umiliki wa ardhi.

Alipongeza jamii za Rendille na Samburu katika wadi za Log logo na Karare kwa kuchukua hatua hiyo mahususi.

Hatua hii ni tunda la uhamasishaji endelevu miongoni mwa jamii za wafugaji ambazo bado zimejikita kwenye tamaduni potovu na taasubi za kiume.

Akizungumzia umuhimu wa hatua hiyo iliyochukuliwa na jamii hizo, afisa wa Wizara ya Ardhi anayesimamia usajili wa ardhi ya jamii katika kaunti za Marsabit na Isiolo John Wanjohi amehakikishia jamii zote juhudi za serikali kuu katika kufaulisha mchakato huo.

Amebainisha kuwa kamati hiyo ya jamii iliyoteuliwa itajukumika na usimamzi wa ardhi hiyo kwa niaba ya jamii.

Naye Naibu wa Kamishna wa kaunti ya Marsabit David Saruni ametaka jamii za wafugaji kuelimisha Watoto wao na pia kutojiingiza katika tabia ya kuuza ardhi kiholela.

Pia ameonya dhidi ya mwanajamii yeyote kushurutishwa kuwa skwota katika mchakato huo.

Sheria za kimataifa hutaka wanawake wote kupewa haki na usawa katika umiliki, urithi, na utawala wa ardhi kama njia pekee ya kuhakikisha usawa wa kijinsia katika umiliki wa ardhi.

Bruno Mutunga
+ posts
Share This Article