Rais William Ruto ametoa wito kwa wanasiasa kutoka pande zote za kisiasa kuweka kando tofauti zao na kufanya kazi pamoja ili kutekeleza ajenda ya maendeleo nchini.
Amesema Wakenya wameachana na siasa za kikabila na wanapendelea mawazo na mipango itakayobadilisha maisha yao.
Rais alirejelea uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 akisema alipata asilimia 25 ya kura katika kaunti 39, ishara tosha kwamba Kenya inaelekea kukumbatia umoja.
“Uchaguzi umepita. Kitu muhimu sasa ni kuungana, kufanya kazi pamoja na kupanga mabadiliko ya nchi hii,” alisema Ruto.
Alitoa matamshi hayo katika Ikulu ya Nakuru alikokutana na wawakilishi wadi 120 kati ya 127 wa chama cha Jubilee.
Wawakilishi wadi hao waliahidi kuunga mkono ajenda ya serikali katika mabunge yao husika ya kaunti.
Naibu Rais Rigathi Gachagua, kaimu kiongozi wa chama cha Jubilee Sabina Chege, mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho Nelson Dzuya, katibu mkuu Kanini Kega na katibu mkuu wa chama cha UDA Cleophas Malalah ni miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo.
Rais Ruto aliwahakikishia wawakilishi wadi hao kwamba serikali ya Kenya Kwanza itaunga mkono mswada wa kuyafanya mabunge ya kaunti kujisimamia ili kuongeza uhuru wake.
“Hii itahakikisha mabunge ya kaunti yanawawajibisha viongozi wa serikali za kaunti na kuboresha uwazi,” aliongeza kiongozi wa nchi.
Kadhalika alikipongeza chama cha Jubilee akikitaja kuwa cha kitaifa na kilicho na wawakilishi kutoka kila sehemu ya nchi.
Rais Ruto alitoa wito kwa viongozi nchini kuwa na ujasiri wa kufanya maamuzi sahihi haijalishi ni magumu kiasi gani.