Mashambulizi ya mahakama: Mahakimu na Majaji walalama

Martin Mwanje
2 Min Read

Baraza Kuu la Chama cha Mahakimu na Majaji nchini Kenya limeelezea mashataka makubwa kutokana na hatua ya wanasiasa kuendelea kuishambulia idara ya mahakama na majaji na mahakimu binafsi. 

Hii ni baada ya kufanyika kwa mkutano kati ya asasi tatu za serikali uliowaleta pamoja Rais William Ruto, Jaji Mkuu Martha Koome na Spika wa bunge la Taifa Moses Wetang’ula.

Mkutano huo ulilenga kuangazia madai kuwa ufisadi umekithiri katika idara ya mahakama na kusaka njia za kukomesha uovu huo.

“Mashambulizi haya ya kusikitisha mno yanaonekana kupangwa kimkakati, kutekelezwa kwa utaratibu na kupigiwa debe na viongozi kutoka mrengo fulani wa kisiasa,” kilisema  chama hicho kikiongozwa na Rais wake Jaji Radido Stephen Okiyo.

“Chama pia kimetambua kuwepo kampeni kali inayofanywa na viongozi hawa kuchochea na kuhamasisha kutoheshimiwa kwa maagizo ya mahakama.”

Jaji Okiyo akitoa mfano wa kiongozi mmoja wa kisiasa aliyechaguliwa na alikusanya na kuongoza genge la watu kuharibu mali ambayo kesi yake bado inaendelea mahakamani mjini Eldoret.

Aidha, chama hicho kimetoa mfano wa mwanasiasa mwingine aliyetoa madai ya ufisadi ambayo hakuyathibitisha dhidi ya jaji mmoja anayeshughulikia kesi moja mjini Nakuru.

“Inavunja moyo kwamba mmoja wale wanaohusika katika kampeini zinazolenga kuipaka tope idara ya mahakama na majaji ni afisa wa mahakama ambaye anapaswa kufahamu taratibu na adabu zinazohusiana na matamshi ya umma kwa kesi zinazoendelea mahakamani,” alisema jaji Okiyo.

Amewataka wanasiasa hasa wabunge na viongozi wa serikali kuu wanaotumia mikutano ya hadhara kuishambulia idara ya mahakama na majaji kuheshimu kiapo chao cha utendakazi.

Chama cha Mahakimu na Majaji kimewahakikishia wanasiasa na Wakenya kuwa wanachama wake hawatatikisika wala kutishika katika kutimiza kiapo chao cha utendakazi.

 

 

 

 

Share This Article