Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amewatahadharisha wafanyabiashara wa Gikombaa dhidi ya wanasiasa wanaowachochea kukataa soko la kisasa wanalojengewa.
Prof. Kindiki alisema kuwa ujenzi wa soko hilo utachukua muda wa miezi michache, ambalo linatarajiwa kuwahifadhi maelfu ya wafanyabiashara.
“Tunawasihi wafanyabiashara 6,300 wa Gikomba watupatie miezi michache kukamilisha ujenzi wa soko la kisasa na mateso ya miaka mingi ikiwa ni pamoja la visa vya moto ikizikwa katika kaburi la sahahu,” alisema Naibu huyo wa Rais.
Aliwashutumu viongozi wa upinzani kwa kueneza siasa duni ya kuwachochea wafanyabiashara, bila kuwapa suluhu kuhusu masaibu yanayowakumba.
“Kuna wanasiasa ambao wanachukua fursa kwa kuwachochea watu kuendelea kuwa maeneo yaliyo na hatari ya kukumbwa na mafuriko na moto. Tunawahimiza wanabiashara kuwa na subira na kuipa serikali fursa ya kujenga soko la kisasa,” aliongeza Kindiki.
Aliyasema hayo siku ya Alhamisi alipokuwa akikagua miradi ya maendeleo katika kaunti ya Kirinyaga, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa soko la kisasa la Mukarara na barabara ya Riakithiga- Ngungu- Kiang’ombe katika eneo bunge la Gichugu.