Wanariadha 9 walioinyakulia Kenya nishani 10 katika makala ya 19 ya mashindano ya Riadha Duniani yaliyokamilika Jumapili iliyopita mjini Budapest, Hungary watatuzwa Ijumaa.
Hafla ya kuwatuza mashujaa hao imeandaliwa na Waziri wa Michezo Ababu Namwamba na itaongozwa na Rais William Ruto katika eneo la Upper Hill.
Faith Kipyegon alinyakua dhahabu mbili za dunia katika mita 1500 na mita 5000 huku Mary Moraa akishinda nishani ya dhahabu katika mita 800, akiwa Mkenya wa kwanza kutwaa ubingwa huo tangu mwaka 2013.
Washindi wa nishani za dhahabu wanatarajiwa kutuzwa shilingi milioni moja kila mmoja huku walionyakua nishani za fedha wakipokea shilingi laki saba unusu na nusu milioni kwa washindi wa medali za shaba.
Walionyakua nishani za fedha kwa Kenya walikuwa Emmanuel Wanyonyi katika mita 800, Beatrice Chepkoech katika mita 3,000 kuruka viunzi na maji na Daniel Simiu katika mita 5,000.
Washindi wa nishani nne za shaba za Kenya walikuwa Beatrice Chebet katika mita 5,000, Faith Cherotich na Abraham Kibiwott katika mita 3,000 kuruka viunzi na maji na Jacob Krop katika mita 5,000.
Kenya ilimaliza ya tano kwa jumla katika msimamo wa medali na ya kwanza barani Afrika.
Hata hivyo, wanariadha wengi walionyakua nishani bado wangali barani Ulaya na bara Asia kushiriki mashindano ya Diamond League.
Baadhi ya washindi wa nishani za dunia mjini Budapest ambao watakosa halfa ya kutuzwa ni pamoja na Beatrice Chepkoech, Beatrice Chebet, Faith Cherotich, Abraham Kibiwott na Emmanuel Wanyonyi.