Waziri wa uwekezaji, biashara na viwanda Salim Mvurya, ametoa onyo kali kwa wawekezaji ambao wameweka leseni za kuhudumu katika vituo spesheli vya kiuchumi humu nchini.
Akizungumza wakati wa kuzindua ujenzi wa kituo cha “Crystal Frozen and Chilled Foods Limited” huko Naivasha, waziri huyo alisisitiza kujitolea kwa serikali kuhakikisha uwekezaji na maendeleo mwafaka kwenye vituo hivyo.
Alisema wawekezaji watakaokosa kuanzisha biashara baada ya mwaka mmoja wa kupata leseni watapokonywa leseni hizo, huku akielekeza mamlaka simamizi ya maeneo spesheli ya kiuchumi kutekeleza hilo.
“Tunampa kila mwekezaji miezi sita kuanzisha biashara la sivyo, leseni itakabidhiwa mwekezaji mwingine.” alisema Mvurya.
Kufikia sasa kampuni 19 zimeonyesha nia ya kuwekeza kwenye kituo hicho ambacho ujenzi wake umezinduliwa leo huko Naivasha ambapo 11 kati yazo zimekubaliwa na kukabidhiwa leseni.
Maendeleo hayo kulingana na waziri yanatokana na mpangilio wa serikali wa kurahisisha utekelezaji wa biashara nchini huku akihimiza wawekezaji kutumia fursa iliyopo.
Mvurya alihimiza wawekezaji pia kushirikiana na jamii za maeneo ambapo viwanda vyao vipo hasa kwa kuwapa kipaumbele katika nafasi za ajira.
Kuhusu malalamishi ya mwekezaji mmoja kutoka Uturuki kukosa kulipa vijana waliokuwa wakimfanyia kazi, Mvurya alisema kwamba serikali inafuatilia suala hilo na ubalozi wa Uturuki nchini.
Kituo spesheli cha kiuchumi cha Crystal Frozen and Chilled Foods Limited kitahusika na uandaaji wa vyakula hasa mboga.