Watu walio na vyeti ghushi vya masomo watalazimika kusalimisha kwa serikali mapato yote yaliopatikana kwa kutumia vyeti hivyo.
Tume ya maadili na vita dhidi ya ufisadi (EACC), imeanzisha uchunguzi dhidi vyeti ghushi vya masomo vinavyomilikiwa na wakenya.
Mwenyekiti wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi Askofu Dkt. David Oginde amesema tume hiyo inasikitishwa na mtindo unaoendelea ambapo watu wanatumia vyeti ghushi kutafuta kazi sio tu katika sekta ya utumishi wa umma lakini pia katika sekta ya kibinafsi.
Akiongea katika kaunti ya Kisumu, askofu Oginde alisisitiza umuhimu wa Wa-Kenya kuzingatia uadilifu kama fadhila kwenye juhudi zao.
“Visa vya umiliki wa vyeti ghushi vya masomo vimeongezeka. Tumepokea ripoti kutoka pembe zote za nchi na katika viwango tofauti vya serikali,” alisema Oginde.
Alisema wakenya wengi wamepata ajira katika utumishi wa umma kwa kutumia vyeti ghushi vya masomo.