Serikali ya kaunti ya Mandera imewaonya wakazi wa eneo hilo dhidi ya kuhujumu miradi ya maendeleo ya kaunti hiyo.
Akihutubia wananchi wakati wa maadhimisho ya siku kuu ya Mashujaa, Gavana wa kaunti hiyo Mohamed Khalif, alitoa wito kwa wakazi wa kaunti hiyo kuishi kwa umoja na kukuza maendeleo.
Khalif alisema wale watakaopatikana wakiharibu miundomsingi ya serikali, watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Akizungumza katika sherehe hizo, kamishna wa kaunti ya Mandera Amos Mariba, alitoa wito wa kudumishwa kwa amani na ushirikiano katika kaunti ndogo zote za eneo hilo.
Aidha Mariba aliwahimiza wananchi kushirikiana na maafisa wa usalama, huku akiwataka kutoa habari kuhusu wale wanaohujumu miradi ya serikali katika kaunti hiyo.
Sherehe za mashujaa katika kaunti hiyo ziliandaliwa katika uwanja wa Takaba, ulioko Mandera Magharibi.