Wanaoendesha biashara ya gesi bila leseni mashakani

Tom Mathinji
1 Min Read
Katibu katika wizara ya kawi,Alex Wachira.

Serikali imetoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanoendesha biashara ya gesi bila leseni, huku wakitakiwa kuhakikisha wanazigatia sheria zilizopo.

Akizungumza katika kaunti ya Nyeri siku ya Jumamosi, katibu katika wizara ya kawi Alex Wachira, alisema wale ambao watapatikana wakikiuka taratibu zilizopo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Hatutanyamaza huku mkihatarisha maisha ya wakenya. kupitia wizara ya usalama, maafisa wa polisi wa kitengo cha kawi, pamoja na halmashauri ya kudhibiti kawi EPRA, tutahakikisha wakenya wako salama,” alisema katibu Wachira.

Alisema kuwa wizara ya kawi itafanya operesheni ya kitaifa kuwasaka wafanyabiashara wanaoendesha biashara ya gesi bila leseni.

“Ikiwa unafanya biashara hiyo bila leseni, funga biashara hiyo haraka iwezekanavyo. La sivyo utakumbwa na madhara makubwa,” alidokeza katibu huyo.

Kulingana na Wachira, serikali haitakubali biashara ya gesi katika maeneo ya makazi ya watu, huku serikali ikijizatiti kuhakikisha mitungi ya gesi inayouziwa wananchi inatimiza masharti ya kiusalama.

Matamshi ya katibu huyo yanajiri siku moja baada ya mlipuko kutokea katika kiwanda kimoja cha gesi Alhamisi usiku katika mtaa wa Embakasi.

Watu watatu walifariki na wengine 280 kujeruhiwa katika mkasa huo.

Website |  + posts
Share This Article