Wanandoa wafa moto Kiambu

Marion Bosire
1 Min Read

Biwi la simanzi limegubika wakazi wa kijiji cha Laare huko Gitithia eneo bunge la Lari kaunti ya Kiambu baada ya mtu na mkewe kuchomeka kiasi cha kutotambulika usiku wa kuamkia leo.

Moto huo unaaminiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme na ulizuka wawili hao wakiwa wamelala.

Peter Kimani Kuria na Mirriam Muthoni walichomeka hadi kufa huku majirani wakishindwa kuuzima moto huo.

Benjamin Gatambia ambaye ni jamaa wa waliofariki alisema kwamba wanaamini moto huo ulisababishwa na tatizo la umeme kwani kwa muda wa mwezi mmoja wamekuwa wakipata matatizo ya stima.

Akithibitisha kisa hicho, chifu wa lokesheni ya Gitithia Samuel Kahoro alisema uchunguzi kuhusu ajali hiyo umeanzishwa na akahimiza wakazi kusalia watulivu wachunguzi wanapotafuta chanzo cha moto huo.

Mwakilishi wa wadi ya Lari Kirenga ameahidi kufuatilia na kuhakikisha kwamba kampuni ya umeme nchini KPLC inatekeleza utathmini wa hasara iliyosababishwa na kupotea kwa umeme kila mara kati ya wakazi wa Laare ili wafidiwe.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *